Mabingwa wa Soka Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ kwa Wanawake Simba Queens kimeanza maandalizi ya mwisho mjini Rabat-Morocco, kwa ajili ya mchezo wa ufunguzi wa Michuano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya wenyeji AS FAR Queens.

Simba Queens itaanza kampani ya kulisaka taji la Afrika Jumapili (Oktoba 30) kwa kucheza mchezo huo wa Kundi A, uliopangw akuchezwa Uwanja wa Moulay Hassan, Rabat.

Meneja wa Simba Queens, Selemani Makanya, amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri na wanasubiri kuanza kupeperusha vyema bendera ya klabu na Tanzania.

Makanya amesema kikosi kilitarajia kuanza rasmi mazoezi jana usiku na wanashukuru hali ya hewa kwa sasa jijini Rabat ni nzuri na inafanana na Dar es Salaam.

“Tunamshukuru Mungu tumefika salama hapa Rabat, safari yetu ilikuwa nzuri na wenyeji wetu kutoka Chama cha Soka Morocco walitupokea vizuri, hakuna changamoto yoyote tuliyokutana nayo, tunaamini kila kitu kitaenda vizuri, ” amesema Makanya.

Meneja huyo ameongeza anafurahi kuona kila mchezaji aliyesafiri hapa ana shauku kubwa ya kutimiza kile ambacho mashabiki, wanachama na viongozi wa Simba wanachokisubiri.

Simba Queens imepangwa katika Kundi A na itafungua pazia la mashindano haya Jumapili kwa kuwavaa wenyeji AS FAR Queens kuanzia saa 2:00 usiku kwa saa za Morocco sawa na saa 4:00 usiku kwa saa za Tanzania.

Fainali hizo zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), zinafanyika kwa mara ya pili ambapo mwaka jana zilichezwa Misri na Mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns ilifanikiwa kutwaa ubingwa.

Aweso aingia saiti Dar atoa maagizo
Geita Gold FC yatamba kuvunja Rekodi