Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka la Wanawake Tanzania Bara na Afrika Mashariki na Kati Simba Queens, limewasilisha maombi kwa Uongozi wa Simba SC, likitaka kuweka kambi nchini Ghana, kabla ya kwenda Morocco kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mwezi ujao.
Simba Queens ilipata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kutwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ mapema mwezi huu jijini Dar es salaam.
Meneja wa Simba Queens Seleman Makanya amesema wamepeleka ombi hilo kwa Uongozi kwa kuipndekeza nchi ya Ghana, ambako wanaamini itawasaidia kwa upande wa hali ya hewa inayoendana na Morocco.
Makanya amesema timu ikiwa Dar es salaam itacheza michezo ya Kirafiki na timu za vijana za kiume kujiweka sawa, huku wakisubiri jibu la ombi waliloliwasilisha kwa Uongozi.
“Tumewasilisha maombi na tunasubiri majibu kama, tutafanikiwa kikosi kitaondoka mara moja kwenda Ghana au sehemu nyingine,” amesema Makanya
Katika Ligi ya Mabingwa, Simba Queens imepangwa Kundi A na Asfar FC ya Morocco, Green Buffaloes ya Zambia na Determine Girls FC ya Liberia.
Kundi B lina timu za Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini, Bayelsa Queens FC ya Misri na inasubiriwa timu moja kutoka ukanda wa UNIFFAC.
AS FAR Rabat ya Morocco imeingia moja kwa moja kwenye Michuano hiyo kama timu mwenyeji, huku Mamelod Sundowns Ladies ya Afrika Kusini ni washindi wa pili wa COSAFA na imeingia kwa tiketi ya Bingwa Mtetezi wa msimu uliopita.