Uongozi wa Klabu ya Coastal Union, umesema itahakikisha inashinda mechi mbili zilizobaki dhidi ya Azam FC na SimbaSC ili kupata alama sita ambazo zitaihakikishia kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara bila kwenda kucheza mechi za mchujo ‘Play Off.’
Coastal Union itaanza kukipiga dhidi ya Azam FC mwishoni mwa juma hili katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, kisha itaelekea jijini Dar es salaam kumalizana na Simba SC katika mchezo wa mwisho wa kufunga Pazia la Ligi Kuu msimu huu.
Afisa Habari wa Coastal Union Miraji Wandy, amesema wanaziheshimu Azam FC na Simba SC kwa sababu ni timu kubwa na ngumu, lakini wao wamejipanga kuhakikisha wanakamilisha kazi ambayo Wanachama na Mashabiki wa Klabu hiyo wamewatuma, kuhakikisha kuwa timu yao inaendelea kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
“Ni kweli ligi safari hii ni ngumu sana, michezo iliyosalia Coastal Union tulijipanga kuhakikisha tunapata ushindi, imebaki nyumbani dhidi ya Azam na ugenini dhidi ya Simba, tunaziheshimu sana timu hizo, lakini tutahakikisha tunapata ushindi kwenye mechi hizo kama ambavyo huwa tunapata kwenye timu zingine.
“Tunaanza na Azam FC ambaye anatufuata nyumbani, huku atapigika tu kwa sababu ni mechi ambayo mashabiki wanajazana kutupa sapoti uwanjani kubwa na kutushangilia, na itakuwa ya kuagana kwa sababu hatutaonana tena hadi mwakani. Itakuwa kama sherehe, hivyo Azam ajipange, halafu tunakwenda Dar es Salaam kumalizana na Simba SC,” amesema.
Juzi Jumapili (Mei 14) Coastal Union iliichapa Ihefu FC 1-0, katika mchezo wa Mzunguuko wa 28 wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Kwa matokeo hayo, Coastal Union imefikisha alama 33 ikiwa kwenye nafasi ya 10 ambayo bado haijaipa uhakika wa moja kwa moja kuepuka mechi za mchujo, Ihefu ikiwa juu kwenye nafasi ya tisa kwa alama hizo hizo 33.