Uongozi wa Simba SC umeweka wazi kuwa utafanyia kazi mapendekezo ya Benchi la Ufundi kwenye upande wa usajili ili kuongeza wachezaji imara ndani ya timu hiyo kwa msimu ujao.
Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ambaye kwa sasa yuko mapumzikoni nchini Brazil amewaomba viongozi wa timu hiyo kuongeza wachezaji wawili wawili kila idara ili kuongeza nguvu ndani ya kikosi kwa msimu ujao.
Kukamilika kwa usajili ndani ya Simba SC kutamrahisishia Oliveira kwenye utendaji wake katika kupambania malengo kuanzia msimu ujao 2023/24.
Simba SC imepishana na mataji yote iliyokuwa inapambania ikiwa ni pamoja na ligi, Azam Sports Federation, Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikigotea nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 73.
Mwenyekiti wa Bodi ya Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema: “Kwa namna ambavyo tumefanya kwenye ligi hatujapenda kwani malengo yetu hayajafikiwa hivyo ambacho tunakifanya ni kufanyia kazi makosa yaliyopita na kufanya usajili mzuri kwenye kila idara.
“Kikubwa ambacho tunahitaji kwa msimu ujao ni kuwa tofauti na kupata kile ambacho tunahitaji. Usajili wetu ujao tunaamini utakuwa mzuri na tunaamini kila kitu kitakuwa sawa kwani tunaendelea vizuri.”
PANGA LAENDELEA
Wakati huohuo, Simba SC jana Jumanne (Juni 20) ilitangaza kuachana na wachezaji wao Victor Akpan raia wa Nigeria na Mohamed Outtara raia wa Ivory Coast.