Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC leo Jumanne (Februari 16) wataanza safari ya kuelekea mjini Musoma, Mara, tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu, dhidi ya Biashara United Mara.
Kikosi na benchi la ufundi la Simba SC kitaondoka Dar es salaam kwa ndege hadi jijini Mwanza, na kisha kitaendelea na safari kesho Jumatano (Februari 17) hadi mjini Musoma, Mara tayari kwa mpambano huo utakaopigwa Alhamis (Februari 18) Uwanja wa Karume.
Kikosi cha Simba SC jana Jumatatu (Februari 15) kilianza maandalizi ya mchezo huo Uwanja wa Mo Simba Arena, uliopo Bunju jijini Dar es salaam, baada ya mapumziko ya siku moja, kufuatia kutoka safari ya DR Congo walipokwenbda kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa BArani Afrika dhidi ya AS Vita Club.
Kocha mkuu wa Mabingwa hao wa Tanzania Bara Didier Gomes amesema kuwa wanatambua mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa, lakini jambo la kwanza watakalo kwenda lano mjini Musoma, Mara, ni kuhakikisha wanavunaalama tatu muhimu.
“Ni mchezo mgumu kwetu hasa ukizingatia kwamba tutakuwa ugenini, haina maana kwamba itakuwa kazi nyepesi hapana.”
“Nimewaambia wachezaji kwamba tunahitaji kupata pointi tatu wao wameelewa hivyo tutakwenda kupambana ndani ya uwanja kwa hali na mali.” Amesema kocha huyo kutoka nchini Ufaransa.
Simba SC kwenye msimamo wa Ligi Kuu ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 39 itakutana na Biashara United Mara iliyo nafasi ya nne na alama 32.