Baada ya mastaa wa Simba SC kuyeyusha dakika 450 katika mechi tano za ushindani bila kushinda, wataikaribisha Kagera Sugar wakitamba kuhakikisha wanashinda mchezo huo, huku wakitangaza kubebwa na mambo matatu.
Ipo wazi kuwa katika mechi tano walizocheza Simba SC mara ya mwisho kushinda ilikuwa dhidi ya Ihefu wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1, mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, katika mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Barani Afrika waliambulia sare mbili na walipoteza mchezo mmoja huku kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara wakiambulia sare moja na walipoteza Kariakoo Dabi, Simba SC 1-5 Young Africans.
Mchezo wao wa sita unatarajiwa kuchezwa kesho Ijumaa (Desemba 15) Uwanja wa Uhuru, ambao utakuwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar iliyotoka kupoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa kuna mambo matatu katika kikosi hicho ikiwa ni ari kubwa ya wachezaji katika kikosi hicho, juhudi na kujiamini kwenye kutafuta ushindi katika mechi zinazofuata.
“Hatujapata matokeo mazuri kwenye mechi zetu zilizopita lakini kwa sasa kuna mambo mengi yameongeza ikiwa ni ari ya wachezaji ukiangalia kabisa unaona namna wachezaji wanavyojituma kutimiza majukumu yao.
“Pili ni juhudi kila mmoja anaonesha namna gani kuna kiu kubwa ya kupata ushindi jambo lingine ni ari mpya katika kikosi mapambano bado yanaendelea mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,” amesema Ally.