Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na Wawakilishi wa Afrika Mashariki kwenye Michuano ya Kimataifa Simba SC, wanatarajiea kuendelea na safari ya kuelekea Morocco leo Jumanne (Februari 22), baada ya kuwasili nchini Instambul-Uturuki.
Simba SC iliondoka Niamey-Niger jana Jumatatu (Februari 21), baada ya kucheza mchezo wa pili wa ‘Kundi D’ dhidi ya US Gendermarie na kupata matokeo ya sare ya 1-1, Jumapili (Februari 20).
Ikiwa nchini Morocco Simba SC itaweka kambi ya siku nne, kujiandaa na mchezo wa tatu wa ‘Kundi D’ dhidi ya RS Berkane uliopangwa kuchezwa Jumapili (Februari 27).
Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ ikiwa na alama nne, baada ya kushinda dhidi ya ASEC Mimosas mabao 3-1 kisha ikatoka sare ya 1-1 dhidi ya US Gendermarie.
RS Berkane inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama tatu, baada ya kupoteza mchezo dhidi ya ASEC Mimosas kwa mabao 3-1, huku ikishinda 5-3 dhidi ya US Gendermarie.
Wakati Simba SC ikijiandaa kupambana dhidi ya RS Berkane, ASEC Mimosas itaikaribisha US Gendermarie ya Niger mwishoni mwa juma hili mjini Cotonou nchini Benin.