Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, wanatarajia kuanza safari ya kuelekea mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro leo Jumatano (Juni 16), tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Maafande wa Polisi (Polisi Tanzania FC).

Kikosi cha Simba SC kinachonolewa na Kocha kutoka nchini Ufaransa Didier Gomes kitasafiri kwa ndege hadi uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na kisha kitachukua basi hadi mjini Moshi.

Kikosi hicho kilirejea kambini rasmi Juni 8 kuendelea na mazoezi baada ya kumalizana na Ruvu Shooting  Juni 3, Uwanja wa CCM Kirumba ambapo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Ruvu Shooting 0-3 Simba.

Mchezo dhidi ya Polisi Tanzania ulioapangwa kuchezwa Juni 19, Uwanja wa Ushirika, unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kufuatia hitaji la alama tatu muhimu kwa timu zote mbili.

Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es salaam, ubao ulisoma Simba 2-0 Polisi Tanzania hivyo utakuwa ni mchezo wa ushindani kwa sababu Simba inahitaji kulinda rekodi, huku Polisi Tanzania ya Kocha Mkuu, Malale Hamsini inahitaji kulipa kisasi.

Simba SC inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kucheza michezo 27, huku ikimiliki alama 67, na wapinzani wao Polisi Tanzania wako nafasi ya 6 wakiwa na alama 41 baada ya kucheza jumla ya michezo 30.

Mo Dewji: Nitashirikiana na KMKM
Simba SC washindwa kuvumilia, watinga Chamazi