Kikosi cha Simba SC leo Jumatano (Februari 23) kinaanza safari ya kuelekea nchini Morocco kikitokea Uturuki, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa Tatu wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya RS Berkane.
Simba SC ilipumzika mjini Istanbul-Uturuki, baada ya kuwasili ikitokea Niaemy- Niger juzi Jumatatu (Februari 21), ambako ilicheza dhidi ya USGN na kuambulia matokeo ya sare ya 1-1.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za Simba SC, zimeeleza kuwa kikosi cha Mabingwa hao Tanzania Bara kitaondoka kuelekea mjini Casablanca.
Simba SC itacheza dhidi ya RS Berkane Jumapili (Februari 27), huku ikiongoza msimamo wa ‘Kundi D’ kwa kufikisha alama 04, ikifuatiwa na ASEC Mimosas ya Ivory Coast yenye alama 03 sawa na RS Berkane huku USGN ikiburuza mkia kwa kuwa na alama moja.