Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC leo Ijumaa (Januari 08) wataanza harakati za kusaka taji la Mapinduzi 2021, kwa kucheza dhidi ya Chipukizi ya Zanzibar, mishale ya saa kumi jioni katika uwanja wa Amaan kisiwani Unguja.

Simba SC ambao wana ari ya kupambana baada ya kuwang’oa FC Platinum kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa jumla ya mabao manne kwa moja, huku wakitinga hatua ya makundi ya michuano hiyo, watahitaji kusaka alama tatu mbele ya wenyeji wao Chipukizi FC, ambao tayari wameshapoteza mchezo wa kwanza wa Kombe la Mapundizi dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kikosi cha Simba SC kitashuka dimbani pasina kocha wake Sven Vandenbroeck, ambaye imethibitika ameachana na klabu hiyo, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati yake na uongozi wa mabingwa hao wa Tanzania bara jana jioni.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa Simba SC baada ya kuachana na kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji zimeeleza kuwa, kocha msaidizi Seleman Matola atakaimu nafasi ya kocha mkuu katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, huku ikisubiriwa kutangazwa kwa kocha mpya.

Katika mchezo dhidi ya Chipukizi, kikosi cha Simba SC huenda kikaundwa na wachezaji ambao hawakutumika kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe.

Kikosi kinachotarajiwa kupangwa dhidi ya Chipukizi, langoni huenda akaanza Beno Kakolanya aisaidiwa na wachezaji wengine kama Thadeo Lwanga, Benard Morrison, Mzamiru Yassin, Hasaan Dilunga, Gadiel Michael, David Kameta, Kennedy Juma na Ibrahim Ajibu.

Dube anahesabu siku Azam FC
Young Africans kujiuliza kwa Namungo FC