Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umesema utachukua hatua za kisheria dhidi ya Orlando Pirates, kufuatia kauli chafu zilizotolewa na Kocha wao Mandla Ncikazi.
Kocha Ncikazi alizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo dhidi ya Simba SC Jumapili (April 17), na kueleza namna walivyosikitishwa na maamuzi ya mchezo huo, pamoja na walivyopokewa wakati wakiwasili Dar es salaam-Tanzania.
Afisa Mtendaji MKuu wa Simba SC Barbara Gonzalez amesema: “Tutachukua hatua dhidi ya Orlando Pirates na sio tu kupitia CAF, bali juhudi za kidiplomasia pia kwa sababu kauli za kashfa hazikubaliki, hii si kwa Simba SC pekee bali Tanzania kwa ujumla,”
“Lazima tuwathibitishie Simba SC ni klabu kubwa na yenye kuheshimika zaidi na sio propaganda wanazozizusha kwetu na hata kwa taifa letu.”
Alipozungumaza na Waandishi wa Habari Kocha Mandla Ncikazi alisema: “Media zenu zote hapa zinaenda kudanganya na kuandika uongo, semeni ukweli, Simba hakustahili kushinda, Simba wamebebwa, hawajatutreat vizuri tangu tumefika, penati waliyopewa hawakustahili, VAR imewekwa lakini haijatumika katika maamuzi”
“Kwa nini mnafanya haya kwa Waafrica wenzenu? Je tutainua soka la Africa kwa namna hii ?! Na tunatoka hapa tukijisifu Simba kashinda, Simba hawajashinda referee ndiye amefanya Simba washinde, Kama kweli Simba ni mabingwa wa kuhonga katika soka, ikibainika wanahonga mpaka waendesha (VAR) tutafika (CAF), mpaka (FIFA) tena wanaweza fungiwa mechi za Confederations of African Football (CAF)”
“Mliyotufanyia hapa kuanzia Airport, Stadium hadi hotelini, Je mtafurahi tukiwafanyia haya pia mkija South Africa ? Tunarejea nyumbani kujipanga sisi hatutalipiza”
Simba SC italazimika kulinda ushindi wake wa 1-0, ama kusaka ushindi zaidi katika mchezo wa Mkondo wa pili ugenini Afrika Kusini siku ya Jumapili (April 24), ili kupata tiketi ya kutinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kwa upande wa Orlando Pirates italazimika kusaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri na kuelendelea, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.