Pamoja na kubakiza michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa klabu ya Simba SC umesema timu yao haitotumia nguvu kumaliza ligi kwani inapaswa kujipanga tayari kwa msimu ujao.
Simba SC imebakiza mechi dhidi ya Ruvu Shooting, Polisi Tanzania na Coastal Union.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba SC Ahmed Ally, amesema kikosi chao kitakamilisha ligi kwa mechi zilizobaki bila papara kwa kuwa tayari wameshajiandaa kisaikolojia kuwa wameshindwa kufikia malengo waliyoyatarajia.
Ahmed amesema pamoja na kukubali kutokuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa, watashirikiana na benchi la ufundi kuhakikisha timu inamaliza msimu vizuri kwa heshima.
Amesema mashabiki wameumizwa na matokeo ya msimu huu, wanaheshimu maumivu ya kila mwanasimba na kinachopaswa sasa ni kuangalia malengo ya msimu ujao.
Ameongeza kuwa kukosa ubingwa mfululizo si jambo la kuogopa kwani yanatokana na matokeo ya usajili na maboresho ya msimu ujao ndio jambo la msingi.
“Ukikosea unapata funzo na kujipanga kurekebisha kosa, naamini viongozi watajipanga na kuboresha kikosi chetu, katika mechi zilizobaki timu yetu itacheza kwa utulivu na kukamilisha ratiba,” amesema Ahmed
Simba SC imeshindwa kufanya vizuri msimu huu baada ya kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ huku ikishindwa kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika msimamo, Simba SC inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 64 nyuma ya Young Africans inayoongoza kwa alama 71 wakati Azam FC ipo nafasi ya tatu kwa pointi 53.