Hatimae Klabu ya Simba SC imethibitisha taarifa za uwezekano wa kukutana na baadhi ya klabu za Afrika kwenye mchezo wa hatua ya mtoano Kombe la Shirikisho.
Simba SC wametoa taarifa hiyo, kupitia kurasa za mitandao ya kijamii, huku Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ likitarajia kuchezesha ‘DROO’ ya michezo hiyo ifikapo mishale ya saa nane mchana.
Simba SC inatarajia kukutana na klabu ambazo zilianzia hatua ya awali ya michuano hiyo ambazo ni Gor Mahia (Kenya), Al Ahly Tripoli (Libya), Marumo Gallants (Afrika Kusini), JS Saoura (Algeria), Red Arrows (Zambia), DC Motemba Pembe (DR Congo), GD Interclube (Angola) na Binga FC (Mali).
Mshindi wa jumla katika mchezo wa hatua ya mtoano atatinga hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho.
Simba SC imeingia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy mwishoni mwa juma lililopita jijini Dar es salaam, kufuatia faida ya kufungwa mabao mengi ya ugenini.