Uongozi wa Simba SC umekiri kuihitaji huduma ya Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Msumbaji na klabu ya Al Ahly Jose Luis Miquissone kwa msimu ujao wa 2022/23.
Taarifa za Miquissone zimeshika hatamu juma hili, huku ikielezwa huenda akatolewa kwa mkopo ama kuuzwa moja kwa moja mwishoni mwa msimu huu, kufuatia kushindwa kuingia kwenye mfumo wa Kocha Pitso Mossimane tangu alipomsajili mwanzoni mwa msimu huu akitokea Simba SC.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema wanahitaji huduma ya mchezaji huyo kwa hali na mali, na kama itathibitika kweli Al Ahly wanamuweka sokoni klabu hiyo haitasita kumrudia ili imsajili tena.
Amesema Uongozi wa Simba SC upo tayari kwa lolote kuhusu Miquissone na itaangalia kama kutakua na uwezekano wa kumrejesha kwa kuzingatia masharti ambayo yatawekwa mezani na Al Ahly, kama kweli wanataka kumtoa kwa mkopo ama kumuuza moja kwa moja.
“Hakuna Mwanasimba ambaye hataki kumuona Miquissone akirejea Simba SC, nikuhakikishie hata wapinzani wa Simba SC wanavyosikia taarifa za mwamba huyu kuhusishwa na klabu yetu matumbo yanawawaka moto huko walipo.”
“Ikithibitika kuna ukweli wa jambo hili na Uongozi wa Simba SC ukajiridhisha kwa kuzingatia kanuni na taratibu zitakazowekwa kwenye makubaliano ya kuuzwa kwake, niseme wazi Luis Miquissone atavaa uzi mwekundu na mweupe msimu ujao, ili aendelee kuwatesa na kuwasumbua.” Amesema Ahmed Ally
Luis Miquissone aliuzwa Al Ahly mwanzoni mwa msimu huu sambamba na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama kwenye klabu ya RS Berkane ya Morocco.
Chama tayari amesharejea Simba SC kupitia usajili wa Dirisha Dogo la Usajili mwezi Januari 2022, baada ya kushindwa kuingia kwenye mfumo wa Kocha Florent Ibenge.