Uongozi wa Simba SC umeanza mchakato wa kumrejesha kikosini Kocha wao wa zamani wa Walinda Lango, Milton Nienov ambaye kwa sasa anawatumikia Mabingwa wa Tanzania Bara Young Africans.
Taarifa kutoka ndani ya Simba SC zinadai kuwa viongozi wa Simba SC wameshakubaliana kila kitu na kocha huyo na walikuwa wanasubiri Young Africans icheze mchezo wake wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Azam FC jana Jumatatu (Juni 12).
Mmoja wa viongozi wa Simba SC amesema kuwa kocha huyo raia wa Serbia amemaliza mkataba wake ndani ya Young Africans na tayari wameshafanya naye mazungumzo.
“Ni kweli kuna maboresho makubwa ya benchi la ufundi yatafanyika, wapo ambao wataachwa kuongezwa wapya watakaokuja kushirikiana na kocha wetu mkuu Robert Oliveira (Robertinho) ambaye amewapendekeza kuja kufanya nao kazi,” amesema kiongozi huyo.
Amesema kuchukuliwa kwa Nienov kunatokana na mahitaji ya timu baada ya kuachana na aliyekuwa kocha wao wa makipa Chlouha Zakaria.
“Lakini Simba SC italeta, kocha mpya wa viungo baada ya kuachana na huyu wa sasa, lengo ni kukiimarisha kikosi kwa sababu uongozi umepania kufanya vizuri msimu ujao,” amesema.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Salim Abdallah “Try Gain’, alinukuliwa akisema wanafahamu makosa waliyoyafanya msimu ulioisha hivyo wamejipanga kufanya maboresho makubwa kuanzia kwenye benchi la ufundi.