Kocha mpya wa Simba ni Sellas Tetteh Teivi, raia wa Ghana, pia ni mmoja wa makocha maarufu barani Afrika.

Kwa sasa kocha huyo gwiji barani Afrika, ndiye kocha mkuu wa timu ya taifa ya Sierra Leone na Simba imefanya mazungumzo naye kwa takriban wiki nzima, imefahamika.

Tayari Simba imetenga dau, na kumefanya mazungumzo naye na yenyewe imeshakubali kila kitu, kilichokuwa kinasubiriwa ni kitu kimoja tu, neno “Yes” kutoka kwa Tetteh.

Kocha huyo aliyewahi kuinoa timu ya taifa ya Ghana, ni maarufu kutokana na mambo kadhaa likiwemo lile la kuiongoza timu ya vijana wa Ghana chini ya miaka 23 kucheza Kombe la Dunia mwaka 2013.

Pia aliwahi kuwa kocha wa muda wa timu kubwa ya taifa ya Ghana na wakati akiwa mwanasoka, alicheza kwa mafanikio katika klabu za Great Mao Mao, Zebi na Hearts of Oak kwao Ghana, pia nchini Nigeria alipozitumikia ACB, Julius Bereger na Iwuanyanwu.

mwaka 2009 aliiwezesha timu ya taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20, kutwaa ubingwa wa kombe la dunia kwa kuifunga timu ya taifa ya Brazil kwa changamoto ya penati 4-3.

Habari za uhakika kutoka nchini Ghana kwa rafiki wa karibu wa kocha huyo, zimethibitisha Simba kufanya naye mazungumzo.

“Mazungumzo yao yamefikia pazuri sana, kocha alichelewa kutoka Sierra Leone ndiyo ikawa shida. Lakini leo (jana) atawapa Simba jibu rasmi, mwanzo alitaka kuona ‘profile’ ya Simba.

“Simba wenyewe wamemwambia wanasubiri na leo (jana) ni mwisho, la sivyo wataendelea na plani nyingine,” kilieleza chanzo.

Alipoulizwa Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe kuhusiana na hilo, alionekana kuwa mkali hiyo jana.

“Nafikiri si sahihi kusema vitu nusunusu, tuacheni tumalize kama kweli ni huyo au mwingine mtajua. Sipendi kuzungumzia vitu nusunusu,” alisema Hans Poppe ambaye amekuwa akipambana kuhakikisha Simba inarejea kwenye fomu.

Iwapo Tetteh atachelewa, uhakika kabisa Simba itaenda kwenye mpango C kumyakua kocha wa zamani wa Azam FC, Joseph Omog raia wa Cameroon.

Mpango A ulikuwa ni Kocha Kallisto Pasuwa wa Zimbabwe ambaye amesitisha kuja baada ya timu yake kufuzu CAF.

Chanzo: Saleh Jembe

Robert Emmanuel Pirès Amshurutisha Jamie Vardy
Jordi Alba Atamani Kuona Pedro Akirejea FC Barcelona