Meneja wa Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ Simba SC, Patrick Rweyemamu amesema baada ya wachezaji na benchi la ufundi kuwasili jijini Dar es salaam mapema leo asubuhi, wakitokea mkoani Kigoma, wachezaji watapewa muda wa juma moja na nusu kwa ajili ya mapumziko.
Simba SC jana Jumapili (Julai 25) ilimaliza rasmi msimu wa 2020/21 kwa kuifunga Young Africans bao 1-0, katika mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho, Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Rweyemamu amesema Uongozi umetoa nafasi kwa wachezaji na benchi la ufundi kupumzika kwa muda mfupi, kutokana na msimu mpya wa Ligi na Michuano ya Kimataifa kuwa karibu, hivyo watalazimika kurudi mapema kwa ajili ya kuanza maandalizi.
“Msimu ujao upo karibu sana, hatuna budi kujipa muda mfupi wa mapumziko kama Juma moja ama Juma moja na nusu, na kisha tutarejea kwenye maandalizi.”
“Tunamshukuru Mungu tumemaliza msimu kwa furaha ya kufikia lengo la kutetea mataji yetu mawili, kwa bahati mbaya upande wa kimataifa hatukufikia lengo, lakini bado tunastahili kumshukuru Mungu kwa tulioyapata.” Amesema Rweyemamu muda mchache baada ya kuwasili jijini Dar es salaam akitokea mkoani Kigoma sambamba na kikosi cha Simba SC.
Msimu ujao 2021-22 Simba SC itatetea taji la Ligi Kuu kwa mara ya tano mfululizo na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kwa mara ya tatu mfululizo, huku ikiiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.