Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC leo Al-Khamis watashuka dimbani kupepetana na Mbao FC kwenye mchezo wa mzunguuko wa 35 wa Ligi kuu Tanzania Bara.

Simba SC ambao tayari wameshatwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu, wataingia uwanjani hii leo, wakiwa na kumbukumbu ya ushindi mkubwa wa mabao manne kwa moja walioupata dhidi ya Young Africans mwishoni mwa juma lililopita, kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na kutinga Fainali.

Mbao FC nao wataingia dimbani wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Mtibwa Sugar walioupata juma lililopita jijini Mwanza, kwenye mpambano wa mzunguuko wa 34.

Ushindi huo uliiwezesha klabu hiyo kufikisha alama 35 zinazoendelea kuwaweka kwenye nafasi ya 19 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara huku Simba SC wakiwa kileleni kwa kumiliki alama 81.

Mchezo wa duru la kwanza uliozikutanisha timu hizo mwanzoni mwa mwaka huu jijini Mwanza Uwanja wa CCM Kirumba, Simba ilishinda mabao mawili kwa moja.

Kocha Mkuu wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC Sven Vandenbroeck kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Mbao FC amesema anahitaji kupata alama tatu ili kuendelea kuupa heshima ubingwa wa msimu huu wa 2019/20, ambao wameshautwaa.

Kocha huyo amesema baada ya mapumziko ya siku mbili, kikosi kilirejea kwenye mazoezi jana asubuhi na anaamini nyota wake watakuwa na nguvu mpya ya kusaka ushindi katika mchezo huo dhidi ya Mbao ambayo inahitaji pia pointi ili kujiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja.

“Tunahitaji kumaliza ligi tukiwa na pointi nyingi, hivyo tunaenda kufanya kazi kuhakikisha wachezaji wanatafuta matokeo, tunajua Mbao FC wako katika hali mbaya, lazima wataingia na nguvu,” alisema Sven.

Naye nahodha wa Simba, John Bocco, alisema: “Mbao ni timu nzuri ingawa wako katika nafasi mbaya, hivyo watakuja kutafuta matokeo, lakini kwa upande wetu tunahitaji kukusanya pointi katika michezo yote iliyobakia,” alisema Bocco.

Namungo FC watangaza vita Fainali ASFC
Kagera: Ubunge CCM mchuano mkali, Majimbo Matatu 125 wachukua fomu