Usajili wa Wekundu wa Msimbazi ‘Simba’ umegota kwa Mlinda Lango kutoka nchini Brazili, Caique Luiz Santos da Purificacao, ambaye kama mambo yatakwenda vizuri basi atamwaga wino klabuni hapo, muda wowote kuanzia sasa ili kuziba pengo la Beno Kakolanya aliyetimkia Singida Fountain Gate.
Awali, Simba SC ilikuwa ikitafuta Mlinda Lango mpya wa kigeni baada ya Aishi Manula kufanyiwa upasuaji ambao utamuweka nje kwa zaidi ya miezi mitatu, huku Beno akiachwa na Walinda Lango waliopendekezwa na Kocha Robert Oliveira ‘Robertinho’ ni Caique, Fabien Mutombora na Alfred Mudekereza wote kutoka Vipers SC ya Uganda.
Simba SC imewaweka kwenye mzani Walinda Lango hao na uzito mkubwa kuegemea kwa Caique, ambaye ni pendekezo la kwanza la Robertinho, anayeamini Mbrazili mwenzake atakuja kuziba pengo la Beno na anaweza pia kumuweka nje Manula kama atazubaa baada ya kupona.
Caique mwenye miaka 25, mzaliwa wa mjini Salvador, Brazil, kwa sasa anaichezea Ypiranga RS inayoshiriki ligi ya Campeonato Brasileiro Serie C, sawa na First League ya Tanzania akiwa Mlinda Lango chaguo la kwanza.
Pia, Caique alikuwa Mlinda Lango chaguo la kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kwa wachezaji wasiozidi miaka 20 (U-20) 2016 na 2017, akikishiriki mashindano mbalimbali.
Wakati akiwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Brazil, alikuwa na nyota wengine wanaowika kwa sasa kwenye duniani kama Richarlison wa Tottenham, Douglas Luiz wa Aston Villa, Lucas Paqueta wa West Ham na Gablriel wa Arsenal.
Chanzo kutoka Simba kimeeleza kuwa klabu hiyo imemtumia mkataba nchini Brazil Mlinda Lango huo, na endapo ataridhika basi ataambatana na Kocha Robertinho aliyeko mapumzikoni nchini humo.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Caique, Simba SC imefikisha wachezaji 12 waliotemwa katika kikosi hicho, wakati ikitangaza kuachana na beki Gadiel Michael.
Awali Simba SC iliachana na Erasto Nyoni na Jonas Mkude, ambao walizua maneno kwa wadau wa soka kutokana na nyota hao walivyoitumikia miamba hiyo ya Msimbazi, hasa Mkude, ambaye alidumu kwa miaka 13.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ amesema kuna mambo mengi mazuri ambayo Mkude ameifanyia Simba SC hivyo walipaswa kukaa na kuzungumza naye nini afanyiwe hata kama hawamtaki awepo kikosini. “Mkude wangemuaga vizuri, hata kama ana mapungufu yake, kwa nini wasimuage kama walivyofanya kwa wengine ili kumpa heshima yake? Naamini atapata timu mapema tu,” amesema Batgol