Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, wapo kwenye maandalizi ya mwisho ya safari ya kuelekea nchini Botswana, tayari kwa mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Kwanza.
Mchezo huo wa kuwania kutinga hatua ya Makundi, utachezwa Oktoba 17 mjini Gaborone, ambapo Simba SC watakua wageni wa Jwaneng Galaxy, ambao ni Mabingwa wa Soka nchini Botswana.
Mwenyekiti wa Simba SC Multaza Magungu amesema matayarisho ya safari ya kuelekea Gaborone, Botswana yanakwenda vizuri, na wanatarajia kukodi ndege maalum itakayowafikisha na kuwarudisha kwa wakati.
“Mpaka sasa hatujapanga ni lini tutakwenda, lakini tutakwenda na ndege ya kukodi kwa siku yoyote, tukiamua tunaweza kunyanyuka na kwenda.”
“Kwanza sisi ni kawaida yetu kukodi ndege, siyo wengine wakikodi wanafanya mpaka sherehe,” amesema Mangungu.
Kuhusu wachezaji ambao waliachwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa sababu ya kuwa majeruhi, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na Jonas Mkude ambaye alikuwa na matatizo ya kifamilia, Mangungu amesema wameshapona na wameanza mazoezi na wenzao, huku wakicheza kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Cambiaso Juzi Jumatano (Oktoba 11).
“Kwa mujibu wa madaktari ni kwamba wameshapona majeraha yao, wameanza mazoezi na wamecheza kwenye mechi yetu ya kirafiki juzi,” amesema Kiongozi huyo.
Mpango wa Simba SC kutokuweka wazi siku ya kuondoka nchini, huenda ni mkakati wa kutaka kuwashtukiza wapinzani wao huko nchini Botswana, ikiwa ni sehemu za mbinu za kimchezo.