Uongozi wa Klabu ya Simba SC umewatoa hofu Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, kuhusu kuzibwa kwa nafasi iliyoachwa wazi na Mshambuliaji kutoka nchini Serbia Dejan Georgejevic.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Nogometni klub Domžale ya nchini Slovenia, alitangaza kuvunja mkataba juma lililopita akiwa visiwani Zanzibar kwa madai ya kushindwa kutimiziwa mahitaji yake kimkataba.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema kwa sasa wapo katika mchakato wa kumalizana na Dejan ili waachane kwa wema, kufuatia muhisika kusisitiza mkataba wake uvunjwe.
Amesema kutokana na hali hiyo ni wazi Simba SC itakua na nafasi moja ya usajili wa Kimataifa, na watahakikisha wanamleta mtu sahihi wakishirikiana na Benchi la Ufundi kupitia Dirisha Dogo la Usajili.
“Jambo muhimu ni kuona nafasi hiyo inazibwa na Mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufumania nyavu, lakini mchakato huo tutashirikiana na Benchi la Ufundi.”
“Tumeshaanza mchakato wa kumsaka Mshambuliaji mwenye sifa ambazo zitatuwezesha kuziba nafasi ya Dejan, hatutafanya makosa katika jambo hilo, ni suala la muda tu.”
“Sina shaka Wanasimba watafurahi na kile ambacho wanakitarajia, huenda ukawa ndio wakati wake umefika.” amesema Try Again.
Hata hivyo Simba SC inahusishwa na mpango wa kumsajili Mshambuliaji Cesar Lobi Manzoki ambaye walimkosa mwanzoni mwa msimu huu, kufuatia kutokuelewana na viongozi wa klabu ya Vipers ya Uganda iliyokua inamiliki.
Kwa sasa Manzoki yupo China akiitumikia klabu ya Dalian Professional kwa mkataba wa miezi minne, ambao utafikia kikomo mwezi Januari 2023.