Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na Wawakilishi wa nchi kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika Simba SC, wamejinasibu kuwa tayari kwa lolote kuelekea mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Red Arrows ya Zambia.
Simba SC itacheza ugenini mjini Lusaka jumapili (Desemba 05), huku ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 uliopatikana Jumapili (Novemba 28), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Msaidizi wa Afisa Habari wa Simba SC Ally Sharty amesema Uongozi wa klabu hiyo umekamilisha taratibu zote za safari ya mjini Lusaka Zambia, huku safari wa kikosi chao ikitarajiwa kuwa leo Ijumaa (Desemba 03).
Sharty amesema Uongozi umejipanga kwa kila hali, ili kuepukana na changamoto zitakazojitokeza watakapokua ugenini mjini Lusaka, tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Kombe la Shirikisho Afrika.
“Tunajua mazingira ya soka la Afrika, mara nyingi unapokua ugenini mambo mengi yanaweza kujitokeza, hivyo Uongozi umejipanga kukabiliana na changamoto.”
“Lengo letu ni kupata ushindi ugenini, tunaamini kikosi chetu kina uwezo wa kufanya hivyo, kwa sababu tuna kiu ya kuendelea kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.” amesema Sharty.
Katika mchezo wa Jumapili (Desemba 05), kikosi cha Simba SC kitalazimika kusaka ushindi ama matokeo ya sare ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya Makundi, huku wenyeji wao Red Arrows wakihitaji ushindi wa mabao 4-0 na kuendelea.