Kikosi cha Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC leo Jumanne (Oktoba 04) kinaanza maandalizi ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Angola Premeiro De Agosto.
Simba SC itaanzia ugenini Estádio França Ndalu mjini Luanda-Angola Jumapili (Oktoba 09), kabla ya kumalizia nyumbani Uwanja wa Benjamim Mkapa jijini Dar es salaam Jumapili (Oktoba 16).
Taarifa kutoka Simba SC zinaeleza kuwa, kikosi cha Simba SC kinaanza mazoezi ya kuelekea mchezo huo, huku kikiwakosa wachezaji watatu Peter Banda, Shomari Kapombe na Jimmyson Mwanuke ambao ni majeruhi.
Katika hatua nyingine, Simba SC imethibitisha kikosi kitaondoka Alfajiri ya Jumamosi (Oktoba 8) kuelekea mjini Luanda-Angola kwa ndege maalumu ya kukodi, tayari kwa siku ya mchezo wa Jumapili (Oktoba 9).
Simba SC ilitinga hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kufuatia ushindi wa jumla wa 4-0 dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Malawi Nyasa Big Bullet, huku Premeiro De Agosto inayomikiwa na Jeshi la Angola, ikipata nafasi hiyo kwa kuitoa Red Arrows ya Zambia kwa ushindi wa jumla wa 2-1.