Hali ya kiafya ya Mlinda Mlango chaguo la kwanza la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Aishi Salum Manula imeendelea kuimarika baada ya kupata matibabu kwenye Hospitali ya Kairuki, jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Simba SC, kupitia ukurasa wao wa Instagram, Manula aliumia jana Jumatatu (Machi Mosi) akiwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Tanzania, uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Haji Sunday Ramadhan Manara ametoa taarifa za kuendelea vyema kwa Mlinda Mlango huyo sanjari na kuruhusiwa kutoka hospitali mapema hii leo.
“Taarifa njema kutoka Simba SC ni kuwa kipa wetu Aishi Manula ameruhusiwa kutoka hospitali ya Kairuki.” Amesema Manara
Manara pia ameongeza kuwa Manula atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaosafiri kuelekea Sudan hapo kesho kwa ajili ya kuwavaa Al Merrikh Jumamosi Machi 6, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
“Anaendelea vizuri na tunaamini atakuwa amepona kabla ya mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merreikh ya Sudan.” Ameongeza Manara
Kabla ya taarifa ya Manara, Daktari Mkuu wa kikosi cha Simba SC Yassin Gembe aliujuza umma wa Mashabiki wa klabu hiyo, juu ya maendeleo ya Aishi Manula kwa kuwataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kutokuwa na wasiwasi dhidi ya mlinda mlango huyo.
“Napenda kuchukua nafasi kuwatoa hofu wapenzi na Mashabiki na Wanachama wa klabu ya Simba kutokana na majeraha aliyopata kipa wetu Aishi Manula siku ya jana, mpaka ninaandika haya muda huu hali yake inazidi kuimarika vizuri”
“Kilichotokea Uwanjani ni kwamba jana alipoteza fahamu baada ya kugongana na mchezaji wa timu ya JKT Tanzania wakati anarukia mpira, kwa hiyo tulimkimbiza Hospital ya Kairuki na tulipata huduma nzuri ambapo alifanyiwa vipimo vyote vinavyohitajika’’
“Hivi ninavyozungumza Aishi Manula anaendelea vizuri kabisa tunasubiri tu uchunguzi wa mwisho wa madaktari bingwa na nina imani atapata ruhusa muda si mrefu, kwa hali hivi ilivyo tuzidi kumuombea dua na hapana shaka atakuwepo kwenye mchezo ujao dhidi ya El Merrikh’’ Ni maelezo aliyoyatoa Daktari Gembe kabla ya taaria ya Manula kuruhusiwa kutoka hospitali.