Na Said Miraj

Kuna watu husubiri timu zipate matokeo mabaya ili wasababishe vurugu katika vilabu vya michezo nchini Tanzania hasa ‘Soka’. Mara nyingi watu hawa huwa hawaonekani wakati wa mafanikio.

Hawa wanataka kutuaminisha kuwa, hakuna timu isiyopoteza ndani na nje ya Uwanja katika Dunia hii, lakini ukweli ni kwamba hakuna Timu isiyopoteza mchezo wala kufekli katika biashara zake nje ya Uwanja, na Simba SC ni miongoni na timu hizo!

Kwa nini hatutaki kuziheshimu timu nyingine na kuamini kwamba tunapojipanga na wenzetu wanajipanga, tena maradufu! Na ndio maana kuna kupanda na kushuka katika mchezo wa Soka.

Kutarajia mafanikio ya ushindi kwa kutwaa mataji kwa misimu yote, ni sawa na kuwadharau wapinzani! Simba SC imepoteza mataji yake kwa msimu mmoja, baada ya kufanya vizuri kwa misimu minne mfululizo, lakini kuna baadhi watu wameanza kupiga kelele hadi zinakaribia kupasua Ngoma za Masikio, kwa nini watu hawa walikaa kimya kwa miaka minne wakati timu ikifanya vizuri ndani na nje ya Uwanja?

Hii inadhihirisha kwamba, watu hawa wanakosa hata shukurani kwa kazi iliyofanywa kwa miaka minne na kuifikisha Simba SC mahali ambapo hakuna timu yoyote ndani ya Tanzania imefika! Baas, hata hilo hawalioni?

Jee! tusingelifanikiwa kuingia katika mashindano ya kimataifa kwa mwaka huu baada ya kukosa makombe ingelikuwaje? Pamoja na mapungufu yaliyopo katika klabu, bado Simba SC ni nembo ya Tanzania kisoka katika medani za kimataifa kwa takriban misimu minne mfululuzo, hata hili hawataki kuliheshimu?

Ntibazonkiza kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara 2022/23

Maneno yanayoendelea sasa kutoka kwa baadhi ya watu, tena wengine ni viongozi wa sasa na wa zamani, ni sawa na ukosefu wa Busara na Hekima kwa Wanasimba wote, na zaidi ni kuonyesha tabia ya kutokuthamini jitihada.

Huku ni kukosa shukurani hata kwa wachezaji wetu ambao wamekua wakijituma kwa kipindi chote na kuiwezesha Simba SC kupata matokeo mazuri na makubwa ndani na nje ya Uwanja.

Sambamba na kutupa furaha Wanachama na Washabiki wa Simba SC, kazi iliyofanyika ndio inayoifanya leo klabu hii kuwa na wapenzi duniani kote, iongoze katika Mitandao ya Kijamii kwa kuwa na  wafuatiliaji wengi, wanachama waweze kuchangia fedha za ujenzi wa Uwanja, kujaza Uwanja kila Simba inapocheza, kushangilia kwa aina yake hadi kuwa miongoni mwa klabu inayosifika kwa washabiki wake kuhudhuria Viwanjani wakati timu yao inapocheza.

Washabiki hawa ndio hununua vifaa vya Michezo vya Klabu kama jezi na kadhalika na kuongeza pato la klabu, leo kila mtu anatamani kuwekeza ndani ya Simba SC, kila mchezaji anatamani kucheza Simba SC, hata Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ linajivunia kwamba timu ya Simba SC ndio inaangaliwa zaidi katika Kurasa zao za Mitandao ya Kijamii, tunataka nini Zaidi?

Kuna miaka kadhaa huko nyuma tulipata Ubingwa wa ndani, lakini  hatukufika popote Kimataifa, Jee ilitujengea heshima kama tuliyonayo sasa?

Ila, tulipo sasa Simba SC tutashiriki Michuano ya Kimataifa, licha ya kupoteza Taji la Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, na hii inatokana na heshima tuliojijengea CAF kwa kuwa na alama nyingi miongoni mwa nchi ambazo zitapeleka timu nne msimu ujao. Tukubali Tukate hili limefanywa na Simba SC.

Leo hii, Simba SC ni miongoni mwa vilabu 15 Bora Barani Afrika, nani mwengine katika Ukanda wa Afrika Mashariki kama sio Simba SC? Kwa hakika mambo ni mengi, Wadau wa Simba SC tulishasahau Siasa za kinafiki katika Soka kwa misimu minne, sasa mbona mnataka kuturudisha nyuma?

Watu wa namna hii ni kama Fisi wanaosubiri mkono ukatike! TUWE MAKINI WATU HAWA!

Kusema tusemeni, ila tuweke akiba ya maneno. KUNA WENGINE NI MAFISI WA MPIRA, ‘AKILI ZA KUAMBIWA CHANGANYA NA ZAKO’.

SIMBA NGUVU MOJA.

Novak Djokovic chali French Open
Jemedari Said: Waliosajili Simba SC walipaswa kufukuzwa