Kikosi cha Simba SC kimeendelea kujifua kuelekea mechi ya Mkondo wa Pili ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika itakayochezwa kesho Jumapili (Oktoba Mosi) dhidi ya Power Dynamos kwa Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho kuweka mkazo zaidi kwa wachezaji wake kuwa na shabaha wanapofika langoni.
Katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mo Arena, Dar es Salaam, kulikuwa na idadi kubwa ya magoli madogo ambayo yalisambazwa Uwanjani na Robertinho aliwataka wachezaji wake kupiga mipira kuelekea katika magoli hayo.
Mazoezi hayo yameonyesha wazi hataki makosa yaliyofanyika katika mechi ya kwanza iliyochezwa Septemba 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola yanajirudia kwa wachezaji wakiongozwa na Mshambuliaji, Jean Baleke kukosa mabao mengi ya wazi.
“Kila kocha ana mbinu zake za ufundishaji kila siku, huwezi kufundisha vilevile kila siku, mara nyingi mwalimu bora ni yule anayetengeneza aina tofauti tofauti ya ufundishaji na mbinu kutokana na mapungufu yanayojitokeza na aina ya mpinzani unayekwenda kucheza naye,” amesema Robertinho.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema wachezaji wao wako katika hatua ya mwisho ya kukamilisha maandalizi kuelekea mechi hiyo lakini wameonyesha kuwa na hamu na mchezo wenyewe.
“Hali ya kikosi iko shwari na wachezaji wetu wanamzuka, wana hamu kubwa na mchezo wenyewe ili wakatimize lengo la kutinga makundi ambapo sisi kwetu Simba SC wala si habari kubwa sana kuingia hatua hiyo,” ametamba Ahmed.
Wakati huo huo, kikosi cha Power Dynamos kilitua nchini juzi Alhamis (Septemba 28) kwa ajili ya mechi hiyo lakini bila kipa wake namba mmoja, Lawrence-Mulenga ambaye aliumia na kukimbizwa hospitali katika mechi ya Ligi Kuu Zambia iliyochezwa Jumamosi iliyopita dhidi ya Zesco.
Kipa huyo alikuwa shubiri kwa wachezaji wa Simba SC kutokana na kuokoa mashambulizi mbalimbali yaliyoelekezwa katika lango lake na kuifanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Katika mechi hiyo ya kesho Jumapili (Oktoba Mosi) Power Dynamos pia itamkosa beki wake wakati tegemeo, Dominic Chanda ambaye alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo wa kwanza Levy Mwanawasa, Ndola Zambia kwa kumchezea vibaya, Baleke.
Meneja wa timu hiyo, Lombe Chipupu amesema hawana wasiwasi na mechi hiyo kwani wamekuja kushinda.
“Hatuna presha huu ni mpira, tumekuja kushinda, tunajua tupo hapa kwa sababu gani, tunajua tunahitaji kushinda au sare ya juu ya mabao 2-2 ndiyo matokeo yatakayotupeleka mbele tumejipanga kwa hilo,” amesema meneja huyo.