Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, ametuma salamu kwa klabu kubwa zitakazoshiriki michuano inayoandaliwa na CAF, kuwa timu za Tanzania si uchochoro tena wa kupita.
Katika hotuba yake, waziri huyo alizipongeza klabu ya Simba na Namungo kwa kuwezesha soka nchini kukua kimataifa kwa ngazi ya klabu baada ya kufanya vizuri.
Alisema mafanikio hayo kwa pamoja yameipa nchi fursa ya kuingiza klabu nne kwenye michuano hiyo ya CAF; mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho Afrika.
Bashungwa alisema serikali itaendelea kuweka mazingira bora zaidi yatakayochochea mafanikio makubwa zaidi ya mpira wa miguu na michezo mingine katika nyanja za kimataifa.
“Klabu hii imeonyesha soka la hali ya juu katika mashindano hayo, kwani ilizichakaza klabu kubwa barani Afrika kama vile FC Platinum ya Zimbabwe kwa mabao 4-0, Al Merreikh ya Sudan mabao 3-0, As Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 4-1, Al Ahly ya Misri bao 1-0 na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini 3-0,” alisema Bashungwa.