Uongozi wa Simba SC umefunguka sakata la Kiungo Kutoka nchini Nigeria Nelson Okwa ambaye ametoa kauli tata siku chache baada ya kuthibitishwa kuachwa na Klabu hiyo, katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya 2023/24.

Okwa alisajiliwa Simba SC msimu uliopita 2022/23 akitokea Rivers United ya kwao Nigeria, lakini alishindwa kuonesha uwezo wake na kuepeleka kuuzwa kwa mkopo Ihefu FC wakati wa Dirisha la Usajili mwezi Januari 2023.

Kiungo huyo amesema pamoja na kuthibitishwa hadharani kuwa hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC, bado Uongozi wa Klabu hiyo haujamlipa sehemu ya fedha yake kama fidia ya kuvunjwa kwa mkataba wake.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema tayari wameshamalizana na nyota huyo na hawana muda wa kubishana na mchezaji ambaye ameshindwa kuonyesha kiwango chake na hata alipopelekwa kwa mkopo Ihefu FC aliendelea kuthibitisha ameshindwa.

“Kama kweli Okwa au kuna mchezaji ambaye tumemuacha anaidai Simba SC basi niwaombe waende kushtaki katika mamlaka husika, ninaimani kuwa hakuna mchezaji anadai kwa wale tuliowaacha,” amesema Ahmed.

Amesema baada ya wiki hii kukamilisha zoezi la kuwapa asante wachezaji ambao hawataendelea nao kwa msimu mpya wa 2023/24, watatangaza rasmi benchi la ufundi kwa wale watakaoziba nafasi ya walioondoka halafu usajili wa wachezaji wapya na badae wataeleza ni wapi wataenda kuweka kambi.

Taarifa zilizopo hadi sasa ni kwamba hadi sasa kuna nchi tatu ambazo ni Canada, Uturuki na Afrika Kusini, ambapo Simba SC iko kwenye mchakato wa wapi waende kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.

AC Milan yajitosa tena kwa Loftus-Cheek
Young Africans yakanusha kufungiwa FIFA