Mabingwa wa Soka Tanzana Bara Simba SC wamemalizana na klabu ya RS Berkane na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama ambaye anahusishwa na mpango wa kurejea Msimbazi mwezi huu.
Dirisha Dogo la Usajili kwa Tanzania Bara linatarajiwa kufungwa rasmi kesho Jumamosi (Januari 15), na klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza zimetumia nafasi hiyo kuboresha vuikosi vyao.
Simba SC ipo hatua za mwisho katika usajili wa Chama na muda wowote nyota huyo wa nchini Zambia atatua kuungana na timu hiyo kuimarisha timu hiyo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano iliyopo mbele yao.
Taarifa kutoka ndani ya Simba SC zinaeleza kuwa Chama ni miongoni mwa wachezaji ambao wameongezwa katika usajili ya dirisha dogo na anatarajiwa kuungana na wachezaji wenzake katika kikosi cha timu hiyo ambacho jana Alhamis (Januari 13) kilitwaa Ubingwa wa Mapinduzi 2022.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzales ambaye yuko visiwani Zanzibar, alipoulizwa kuhusu nyota huyo hakutaka kuweka wazi na kudai kwamba, hivi karibuni watategua bomu katika usajili wao wa dirisha dogo unaotarajiwa kufungwa kesho Januari 15.
“Mashabiki wanatakiwa kuwa na subira kwa sababu viongozi tumekuwa makini katika usajili wetu wa dirisha dogo nani anakuja wavumilie ndani ya hizi siku mbili tutamtambulisha mchezaji ambaye tumemsajili,” amesema Barbara.
Chama aliuzwa RS Berkane mwanzoni mwa msimu huu akitokea Simba SC, lakini mazingira tofauti aliyokutana nayo Morocco yanatajwa kuwa sababu za kushindwa kuonesha uwezo wake kisoka, hivyo ameamua kurejea Tanzania.