Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2020/21 Simba SC leo Jumanne (Novemba 24) mishale ya jioni wataondoka kuelekea Nigeria na msafara wa watu 40, tayari kwa mchezo wa mzunguko wa awali wa michuano hiyo dhidi ya Plateau United.

Simba wataanza safari ya kuelekea Nigeria wakitokea jijini Arusha ambako waliweka kambi ya siku tatu, baada ya kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ya Tanga na kuibuka na ushindi mnono wa mabao saba kwa sifuri.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imeeleza kuwa msafara wa mabingwa hao wa Tanzania bara utaondoka na ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kupitia Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Msafara huo utapitia mjini Addis Ababa – Ethiopia na kisha utaendelea na safari ya kuelekea mjini Lagos, Nigeria kabla ya kuanza mwendo wa kwenda kwenye mji wa Jos, ambako ndipo mchezo dhidi ya Plateau United utapigwa siku ya ijumaa (Novemba 27).

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji amesema msafara wa kikosi cha Simba utakapowasili mjini Lagos, utatumia usafiri wa ndege ya kukodi hadi mjini Jos.

“Lengo la klabu msimu huu ni kufika mbali, kwa mikakati tuliyoiweka na maandalizi tunayoyafanya tunaamini tutatimiza malengo yetu na kufanya vizuri kimataifa,” amesema Mo.

Kikosi cha Simba SC kitakachosafiri kuelekea Nigeria.

Wachezaji Coastal Union kuadhibiwa
Kaze kufanya mabadiliko Young Africans