Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na wawakilishi wa nchi katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Simba SC, leo jioni wamefanya mazoezi yao ya mwisho mjini Gaborone, Botswana.
Simba SC ambayo iliwasili Gaborone jana Ijumaa (Oktoba 15) majira ya usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kwa ndege maalum ya kukodi kesho Jumapili (Oktoba 17) itacheza Mchezo wa Mkondo wa Kwanza hatua ya Kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes amesema kuwa, maandalizi ya mwisho ya kikosi chake yamekwenda vizuri na ana matumaini ya kuibuka na ushindi ugenini.
“Tumekamilisha maandalizi ya mchezo wetu wa kesho Jumapili hapa Gaborone, imani yangu wachezaji watapambana na kupata matokeo mazuri,”
“Tumekuja hapa Botswana kupambana ikiwa ni mwanzo wa safari yetu ya kutafuta ushindi utakaotufikisha kwenye malengo yetu ya kufika Nusu Fainali ya michuano ya Afrika.” amesema Gomez.
Msimu uliopita Simba SC ilifika hatua ya Robo Fainali, na ilitolewa kwa jumla ya mabao 4-3 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Africans.
Baada ya mchezo wa kesho Jumapili (Oktoba 17) kikosi cha Simba SC kitarejea Dar es salaam kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Mkondo wa Pili dhidi ya Jwaneng Galaxy utakaorindima Oktoba 24, Uwanja wa Benjamin Mkapa.