Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wamerejea Jijini Dar es salaam wakitokea Cotonou-Benin ambako walikabiliwa na mchezo wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Jumapili (Machi 20).

Simba SC ilipoteza mchezo huo wa Mzunguuko watano wa ‘Kundi D’ kwa kuchapwa mabao 3-0, hali iliyopelekea kuiweka timu hiyo na Msimbazi katika mazingira ya kuhakikisha inashinda dhidi ya USGN ya Niger ili itinge hatua ya Robo Fainali.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally alizungumza na waandishi wa habari na kuelekeza matarajio yao kuelekea mchezo dhidi ya USGN utakaopigwa Uwanja Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam April 03.

“Lengo lilikua ni kushinda mchezo wetu dhidi ya ASEC Mimosas ili tufuzu tukiwa ugenini lakini ilishindikana, sasa tuna lengo la pili na la mwisho la kuhakikisha tunashinda hapa nyumbani dhidi ya USGN, tunaamini inawezekana.”

“Zaidi ya Mara mbili tumeshafanikiwa kufuzu tukiwa hapa nyumbani, hilo linawezekana kwa sababu kila mmoja katika kundi letu anashinda nyumbani kwao, hivyo nyumbani kwetu sisi ni sehemu ambayo USGN anakuja kupasuaka. hilo sina shaka nalo hata kidogo.”

“Niwaambie wanasimba mchezo wetu utakua April 03 na utachezwa saa moja kamili usiku, kwa hiyo kila mwana simba anapaswa kujiwekea dhamira anapaswa kuja uwanjani siku hiyo.”

“Tumeomba CAF watuongezee mashabiki siku hiyo, kama watatuongezea tutashukuru na kama wataendelea kutupa idadi ile ile ya Mashabiki 35000 nayo itakua sawa, ila kwa vyovyote itakavyokuwa ni muhimu kwa mwanasimba kujiwekea lengo la kufika Uwanjani siku hiyo ili kuipa nguvu timu yake.”

“Hatma ya kwenda Robo Fainali ipo mikononi mwetu sisi wenyewe, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kushiriki katika hili ili tujitimizie kile ambacho tunakikusudia.” Amesema Ahmed Ally

Simba SC itacheza dhidi ya USGN Uwanja wa Benjamin Mkapa April 03, huku ASEC Mimosas ikisafiri kuelekea mjini Berkane-Morocco kupambana na RS Berkane.

Msimamo wa ‘Kundi D’ hadi sasa ASEC mimosas inaongoza ikiwa na alama 09, ikifuatiwa na RS Berkane yenye alama 07 sawa na Simba SC huku USGN ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 05.

Waziri Mkuu Majaliwa akutana na Waziri Mkuu wa Qatar
Tanzania kuungana na nchi za SADC kuadhimisha siku ya ukombozi