Mabingwa watetezi Tanzania Bara Simba SC wameahidi ushindi kwa mashabiki na wanachama wao dhidi ya Ruvu Shooting, katika mchezo utakaochezwa baadae leo Jumatatu Oktoba 26.

Simba SC watakua wenyeji wa mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam mishale ya saa kumi jioni, huku wakihitaji kurekebisha makosa ya kuangusha alama tatu dhidi ya Tanzania Prisonas, juma lililopita.

Meneja wa Simba SC, Patrick Rweyemamu, amesema wanafahamu kila mchezo wa Ligi Kuu ni muhimu, hivyo wataongeza umakini katika mchezo wa leo kwa sababu malengo yao ni kutetea taji la Ligi Kuu (VPL) wanalolishikilia.

“Ukimaliza mchezo unafunga hesabu, huwezi kubadilisha matokeo, unaanza ukurasa mpya, sasa hivi kiufundi tunaiangalia Ruvu Shooting, ndio mtihani ulioko mbele yetu, tumeshaanza kuipigia hesabu, tujue tutamalizana nao vipi,” amesema Rweyemamu.

Wakati huo huo Kocha Mkuu wa Simba SC Sven Vandenbroeck amesema kuwa, anaamini mchezo wa leo jumatatu Oktoba 26, utakuwa na ushindani mkubwa ila wanahitaji alama tatu muhimu.

“Ni mchezo mgumu na wenye ushindani mkubwa, imani yangu ni kwamba wachezaji wanajua kwamba mchezo uliopita tumepoteza, ila tutafanya vizuri kwenye mchezo wetu dhidi ya Ruvu Shooting.

“Mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani kuipa sapoti timu yao na tuna amini kwamba tutafanya vizuri,” amesema.

Msimu uliopita walipokutana Uwanja wa Mkapa mchezo wa mwisho, Simba ilikubali sare ya kufungana bao 1-1 hivyo leo kazi itakuwa kubwa kwa timu hizi mbili.

Mtangazaji wa TBC Elisha Elia kuzikwa kesho Mbeya
NEC yakanusha madai uwepo wa vituo hewa vya wapiga kura