Mabingwa Ligi Kuu Tanzania Bara mara tatu mfululizo Simba SC, leo wamelazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji, Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Sare hiyo ya tatu mfululizo na ya bila mabao, inaifanya Simba SC ifikishe alama 81 baada ya kucheza mechi 34 na sasa inawazidi alama 19 Azam FC na 20 Young Africans SC wanaofuatia nafasi ya pili na ya tatu.
Baada ya mchezo huo uliochezeshwa na Mwamuzi Hamdani Said wa Mtwara aliyesaidiwa na Credo Mbuya wa Mbeya na Abdallah Lisakasa wa Lindi, kikosi cha Simba SC kimekabidhiwa Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu ambalo litakuwa la kwao moja kwa moja kutokana na kulitwaa kwa mara ya tatu mfululizo.
Hilo linakuwa taji la 21 la Ligi Kuu kwa Simba SC baada ya awali kubeba taji hilo mwaka 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2010, 2012, 2018 na 2019.
Vigogo, Young Africans SC wanabaki kuwa mabingwa mara nyingi zaidi wa taji hilo, 26 katika misimu ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017.
Timu nyingine zilizobeba taji hilo ni Cosmopolitans ya Dar es Salaam 1967, Mseto SC ya Morogoro 1975, Pan African ya Dar es Salaam 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986, Coastal Union ya Tanga 1988, Mtibwa Sugar ya Morogoro 1999 na 2000 na Azam FC 2014.
Kikosi cha Namungo kilikuwa; Nourdine Balora, Miza Christom, Edward Manyama, Stephen Duah, Carlos Protas, Hamisi Khalifa, Hashim Manyanya/Jamal Issa dk73, Steve Nzigamasabo, Bigirimana Blaise/John Kelvin dk31, Lucas Kikoti na Abeid Athumani.
Simba SC; Beno Kakolanya, Haruna Shamte/Hassan Dilunga dk63, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili, Tairone Santos/Gardiel Michael dk52, Said Hamisi, Miraji Athumani ‘Madenge’, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/Cyprian Kipenye dk71 na Francis Kahata/Deo Kanda dk63
Matokeo ya michezo mingine ya mzunguuko wa 34 Ligi Kuu Tanzania Bara iliyocheza hii leo Jumatano.