Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na wanafainali Kombe La Shirikisho (ASFC) Simba SC, wametaja idara wanazotarajia kuziboresha katika kikosi chao kuelekea msimu ujao 2020/21.

Simba SC imejipanga kufanya usajili wa kuboresha kikosi chao ambacho msimu huu kimetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ya mara tatu mfululizo, huku kikionekana kuwa na wachezaji mahiri.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo Haji Sunday Manara, amesema wanatarajia kuongeza wachezaji wasiozidi wanne katika dirisha la usajili ili kukiimarisha kikosi chao kuelekea michuano ya kimataifa, Ligi Kuu na michuano mingine msimu ujao.

Amesema lengo ni kutoharibu uelewano wa wachezaji uwanjani ambao tayari kocha ameutengeneza, hivyo wanachotazama ni kuongeza nguvu kidogo katika idara ya ushambuliaji na safu ya ulinzi.

“Hatuwezi kubadili timu nzima kama Yanga, matarajio yetu ni kusajili mabeki wawili ama watatu na washambuliaji wawili tu ili kuongeza nguvu,” amesema Manara.

“Tutasajili mshambuliaji mmoja wa kimataifa na mmoja wa ndani na kwa upande wa beki ikiwezekana mmoja wa kimataifa na mwingine wa ndani, hatutaki kuwa kama Yanga ambayo msimu ujao unaweza kushuhudia ikisajili wachezaji 15 wapya.”  

Simba SC wataiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Namungo FC ikiwa na tiketi ya kupeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Video: Moto wawaka majimboni, Wadhamini wa Lissu wabanwa Mahakamani
36 wachukua fomu kuwania ubunge jimbo la Bukoba mjini