Baada ya kuwepo uvumi kutoka kwa wadau wa Soka la Bongo juu ya sakata la Moses Phiri kudaiwa kutokuwa na maelewano mazuri na kocha wa kikosi hicho, Roberto Olviera ‘Robertinho’, uongozi wa Simba SC umefungukia sakata hilo kwa kusema kuwa wao hawajui kama kuna ugomvi baina yao.
Phiri aliungana na Simba SC msimu uliopita akitokea Zanaco FC ya kwao Zambia, ambapo aliifungia klabu hiyo mabao 10, nyuma ya Saidi Ntibazonkiza aliyemaliza mfungaji bora baada ya kuifungia mabao 17, akiwa sambamba na Fiston Mayele aliyekuwa akiitumikia Young Africans.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa, pamoja na kuwepo na kelele nyingi mitandaoni dhidi ya kocha wao akihusishwa kutokuwa sawa na Phiri, wao hawajapokea malalamiko kutoka pande hizo mbili hivyo hawana cha kusema kwa sasa.
“Phiri ni mchezaji mzuri, baada ya msimu uliopita kusumbuliwa na majeraha ripoti ya madaktari wetu ilibainisha kuwa kwa sasa ni mzima na yupo tayari kuitumikia klabu, endapo kocha Robertinho akimpanga.
“Kuhusiana na yanayoendelea mitandaoni, sisi hatuna cha kuzungumza maana hadi muda huu hatujapata malalamiko ya wawili hao kutoelewana, jambo ambalo ni uzushi tu huko mitandaoni, ila ninachoweza kusema Phiri ni mchezaji mzuri kiasi kwamba klabu yoyote yenye malengo naye haiwezi kukubali kumuacha kutokana na ubora wake,” amesema Ahmed.