Hatimaye uongozi wa klabu ya Simba umezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu mipango ya kumsajili ama kutokumsajili kiungo mshambuliaji wa Young Africans, Bernard Morrison ambaye amekuwa akitajwa kuhitajiwa Msimbazi kwa ajili ya msimu ujao.
Simba SC imetajwa kwa ziadi ya majuma mawili kuhusu mpango wa kumsajili kiungo huyo ambaye aliingia kwenye mzozo na uongozi wa Young Africans siku za karibuni kabla ya kurejea kundini.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Haji Sunday Manara amesema kuwa Simba wana wachezaji wengi wazuri na hawana mpango wa kumvuta ndani ya kikosi chao kiungo huyo kutoka nchini Ghana.
“Hakuna mpango wa Simba kuzungumza na Morrison, tunatambua kwamba tupo imara na hatuwezi kuzungumza na mchezaji huyo licha ya kwamba yupo vizuri.”
“Ninajua ni mchezaji mzuri ila hayupo kwenye mipango yetu kwa sasa, hayo yanayozungumzwa ni maneno tu hamna kitu kingine,” amesema Haji alipokua kwenye kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM mapema leo Ijumaa.
Luc Eymael: Ni mchezo muhimu sana kwetu
Morrison ambaye ana “mbwembwe” anapokua uwanjani alipata umaarufu mkubwa baada ya kuitungua Simba SC Uwanja wa Taifa, Machi 8 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo Simba ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.