Vinara wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba wameondoka jijini Dar es salaam kuelekea jijini Mbeya, tayari kwa mchezo wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Mbeya City.

Simba wameondoka jijini humo kwa usafiri wa anga, na kesho watapata nafasi ya kufanya maozezi yao ya mwisho kwenye uwanja wa Sokoine ambao utatumika kwenye mchezo wao wa jumapili.

Taarifa iliyothibitishwa na idara ya habari na mawasilino ya klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi jijini Dar es salaam, imeeleza kuwa wachezaji wote wamesafiri isipokuwa majeruhi watatu, kipa Said Mohammed ‘Nduda’, mabeki Shomari Kapombe na Salim Mbonde.

Kikosi cha Simba kitakaa jijini Mbeya kwa ziadi ya siku kumi, kutokana na kukabiliwa na mchezo mwingine wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons, ambao utachezwa Novemba 18 kwenye uwanja wa Sokione.

Hata hivyo benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Joseph Marious Omog, limependekeza kuchezwa mchezo wa kirafiki katika kipindi ambacho Simba watakua wakisubiri mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, na tayari mazungumzo baina ya uongozi wa klabu hiyo kongwe na baadhi ya klabu za soka ukanda wa nyanda za juu kusini yanaendelea, kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kupatikana kwa mchezo huo.

Wakati Simba wakisafiri kuelekea jijini Mbeya, ligi kuu ya soka Tanzania bara itaendelea tena kesho kwa mabingwa mabingwa watetezi, Young Africans kuwa wageni wa Singida United kwenye uwanja wa Namfua mjini Singida, na Ndanda FC wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Michezo mingine ya kesho jumamosi, Kagera Sugar wataikaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Njombe Mji FC wataikaribisha Mbao FC Uwanja wa Saba Saba na Azam FC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Na Jumapili mbali na Mbeya City kuwa wenyeji wa Simba, Lipuli FC nao wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.

35 waitwa kuunda kikosi cha U23
Nape Nnauye aapa kuinyoosha CCM