Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na wawakilishi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Simba SC, wamejinasibu kuwa tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili hatua ya Kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo, utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Jumapili (Oktoba 24) kuanzia saa kumi kamili jioni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo Alkhamis (Oktoba 21), Msaidizi wa Afisa Habari wa Simba SC Ally Shatry amesema, maandalizi ya kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Mkondo wa Pili hatua ya Kwanza yanaendelea vizuri , huku kikosi chao kikiingia kambini chini ya Kocha Mkuu Didier Gomes.
Amesema Tiketi kwa Mashabiki 15,000 walioruhusiwa kuingia Uwanjani siku hiyo zinaendelea kuuzwa, hivyo kwa wale ambao bado hawajakata tiketi hizo wafanye hivyo ili kuepuka usumbufu ama kukosa kabisa.
“Maandalizi ya timu yanakwenda vizuri, tayari wachezaji wameingia kambini kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Wapinzani wetu waliwasili jana, japo wametushtukiza.” amesema Shatry.
Simba SC ilichomoza na ushindi wa mabao 2-0, katika mchezo wa Mkondo wa kwanza uliochezwa mjini Gaborone, Botswana Jumapili (Oktoba 17), na itatakiwa kulinda ushindi huo ama kuongeza ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya Makundi.