Kikosi cha Simba SC kitacheza mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kuwavaa Mabingwa wa Soka nchini Ivory Coast ASEC Mimosas ya, huku ikipanga kuziangalia video za michezo ya mwisho waliyoicheza wapinzani wao ili kujua ubora na udhaifu wao.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Novemba 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam katika mchezo wa kwanza wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Tayari kikosi hicho kimeingia kambini tangu Jumatatu (Novemba 13) kujiandaa na mchezo huo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Daniel Cadena na msaidizi wake, Selemani Matola.
Taarifa kutoka kambini zinaeleza kuwa, Benchi la Ufundi la Simba SC, tayari limepatiwa mchezo huo wa kirafiki wataocheza kabla ya kukutana na ASEC Mimosas.
Mtoa taarifa hizi amesema lengo la kuuomba mchezo huo, ni kocha kuangalia upungufu na kufanyia maboresho ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi hiyo ya nyumbani.
Ameongeza kuwa, pia Benchi la Ufundi na wachezaji wamepanga kufanya kikao sambamba na kuangalia video za michezo ya mwisho ya ASEC Mimosas waliyoicheza ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanapokuwepo ugenini jinsi wanavyocheza.
“Tumepokea taarifa kutoka katika Benchi la Ufundi kuomba mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kukutana na ASEC Mimosas, lengo ni kuona wachezaji wetu kama mafunzo ya kimbinu wameyashika.
“Pia kuwaongezea mechi fitinesi, baada ya kukaa muda mrefu bila ya kucheza mchezo wa mashindano, hiyo itawarejesha mchezoni wachezaji wetu wakati wakijiandaa kucheza dhidi ya ASEC Mimosas.
“Baada ya mchezo huo, Benchi la Ufundi na wachezaji wote watafanya kikao pamoja na kuangalia video za mechi za mwisho ambazo wamezicheza ASEC Mimosas kwa lengo la kuangalia ubora na udhaifu wao,” amesema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzaia hilo, Cadena amesema: “Maandalizi yanakwenda vizuri kuelekea mchezo dhidi ya ASEC Mimosas, ninafurahia kuona kila mchezaji akirejesha morali yake.”