Kaimu Afisa Habari wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ali Shatry amesema Uongozi wa klabu hiyo unasubiri mapendekezo ya Kocha Mkuu Pablo Franco Martin kuhusu maboresho ya kikosi katika usajili wa Dirisha Dogo.
Simba SC inatajwa kuwa kwenye mpango wa kufanya usajili wa wachezaji wazawa na wale wa kimataifa, katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili ambacho rasmi kilianza juzi Jumatano (Desemba 15).
Shatry amesema kumekuwa na tetesi nyingi kuhusu baadhi ya wachezaji wanaohusishwa na Simba baada ya Dirisha Dogo la usajili kufunguliwa, lakini ukweli ni kwamba Uongozi unasubiri maagizo kutoka kwa Kocha wetu Pablo.
“Tunajua kocha wetu anaendelea kukiangalia kikosi, baada ya mechi zetu mbili za mikoani tutakaa na kocha atupe mapendekezo yake”
“Hizo tetesi hata mimi naziona huko mitandaoni lakini muhimu tusubiri tuone kama wachezaji hao watasajiliwa au ni tetesi tu, itafahamika,” amesema ‘Babu Chico’
Jana Alhamis (Desemba 16) taarifa mitandaoni ziliwahusisha wachezaji wawili wa Azam FC Aggrey Morris na Mudathir Yahya kuwa wako mbioni kujiunga na Simba SC.
Pia Mshambuliaji wa Zanaco FC Moses Phiri na kiungo wa RS Berkane Clatous Chotta Chama naye amekuwa akitajwa kuwa mbioni kurejea katika klabu ya Simba SC.
Simba SC imekuwa na mawasiliano na Chama na hata walipokuwa Zambia kwenye mchezo wa marudiano kombe la Shirikisho dhidi ya Red Arrows, walipata wasaa wa kuzungumza na baba yake mzazi, Chama Senior.