Licha ya kutwaa ubingwa wa Tanzania bara kwa mara ya tatu mfululizo msimu huu 2019/20, Simba SC wametangaza njaa ya ushindi dhidi ya Ndanda FC, katika mchezo wa mzunguuko 33 utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Simba SC waliwasili mjinji Mtwara Jana Ijumaa wakitokea Dar es salaam, na leo wanafanya maandalizi ya mwisho tayari kwa mchezo huo, ambao utaanza mishale ya saa kumi jioni kesho Jumapili.
Meneja wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu mtaa wa Msimbazi, Dar es salaam Patrick Rweyemamu, amesema pamoja na kuwa wameshatetea ubingwa, watashuka uwanjani kuikabili Ndanda FC wakidhamiria kupata ushindi na si kukamilisha ratiba.
Rweyemamu amesema kila mchezo kwao ni muhimu na watashuka uwanjani wakifahamu wenyeji wao wanahitaji ushindi ili kujiondoa kwenye janga la kushuka daraja.
“Tunahitaji ushindi, tunahitaji kuupa heshima ubingwa wetu, tutacheza kwa nguvu ile ile ya mwanzoni,” alisema kwa kifupi meneja huyo.
Baada ya mchezo huo, Simba SC wataeelekea Lindi kwa ajili ya kuwavaa Namungo FC katika mchezo wa mzunguuko wa 34 wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja Majaliwa mjini Ruangwa.
Mabingwa hao watakabidhiwa Kombe la ubingwa msimu wa 2019/20, mara baada ya mchezo dhidi ya Namungo FC.
Michezo ya mzunguuko wa 33 wa Ligi Kuu Tanzania Bara inaanza kuchezwa leo Jumamosi (Julai 04/2020).
Kagera Sugar Vs Ruvu Shooting (Kaitaba, Bukoba)
Namungo FC Vs JKT Tanzania (Majaliwa Stadium, ruangwa , Lindi)
Mbao FC Vs Lipuli FC (CCM Kirumba, Mwanza)
TZ Prisons Vs Polisi TZ (Sokoine, Mbeya)
Kesho Jumapili (Julai 05/2020).
Biashara United Vs Young Africans (Karume, Musoma)
Ndanda FC Vs Simba (Nangwanda Sijaona, Mtwara)
Alliance FC Vs Mtibwa Sugar (Nyamagana, Mwanza)
Mbeya city Vs Coastal Union (Sokoine, Mbeya)
Azam FC Vs Singida United (Azam Complex, Dsm)