Hatimaye Uongozi na Bodi ya Wakurugenzi Simba SC umekutana na umekutana na Wanachama wa Klabu hiyo ambao walikuwa wanashinikiza kujiuzulu kwa Mwenyekiti Murtaza Mangungu sambamba na Mwenyekiti wa Bodi, Salim Abdallah ‘Try Again’.
Shinikizo hilo la wanachama kwa viongozi hao liliibuka baada ya kikosi cha Simba SC kupoteza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans kwa idadi kubwa ya mabao (5-1), Novemba 05 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Pande hizo mbili zimekutana jijini Dar es salaam katika Ukumbi wa Gerezani na zimejadiliwa agenda Kuu nne kutoka kwa Wanachama ambazo ni Mpasuko ndani ya Klabu, Timu kufanya vibaya, Mabadiliko ya Katiba na Usimamishwaji wa baadhi ya viongozi wa matawi bila utaratibu.
Baada ya kusikiliza Agenda hizo Uongozi wa Simba SC, kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi Simba SC, Salim Abdallah na Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu wamekubaliana na Wanachama hao Kwanza kuunda Kamati ya maridhiano.
Maridhiano hayo ni pamoja na Uongozi wa Bodi ya Simba SC ukutane na wagombea wote walioshiriki uchaguzi uliopita na kukaa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya Simba SC.
Pia Kikao hicho kimetoa Ushauri wa namna ya kudhibiti kambi kwa maana wanafanya usajili mzuri ila wachezaji huwa hawafanyi vizuri.
Kikao hicho pia kimetazama namna timu yao na baadhi ya wachezaji kuonekana kufanya hujuma, na wamekubaliana wanalifanyia kazi hilo kwa kuzingatia namna bora ya timu kubaki na Uwiyano ‘BALANCE’.
Miongoni mwa makubaliano mengine ni marekebisho ya Katiba na zoezi hilo miongoni mwa wajumbe watarajiwa atakuwepo Advocate Moses Kaluwa ambae alikuwa mgombea wa Uenyekiti Simba SC, na wajumbe wengine watapendekezwa na wanachama waliokuwa wanapinga uongozi watashiriki katika zoezi hilo la kurekebisha katiba ya Simba SC.
Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu amewataka viongozi wote waliosimamishwa bila sababu za msingi warudishwe kwenye nafasi zao mara moja.