Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC wamepoteza mchezo wa kwanza msimu huu 2021/22 dhidi ya Mbeya City leo Jumatatu (Januari 17).
Simba SC imepoteza mchezo huo ugenini Jijini Mbeya katika Uwanja wa Sokoine, huku bao la ushindi la Mbeya City likiwekwa kimiani na Paul Nonga dakika ya 20.
Hata hivyo Simba SC ilipata mkwaju wa penati dakika ya 46 kipindi cha pili, kufuatia beki wa Mbeya City kuunawa mpira eneo la hatari.
Mshambiliaji kutoka DR Congo Criss Mushimba Koppe Mugalu alipewa jukumu la kupiga mkwaju huo lakini alishindwa kuupeleka mpira wavuni, baada ya mpira kugonga mwamba.
Mbeya City imemaliza dakika 90 ikiwa na kikosi pungufu, kufuatia mchezaji Mpoki Mwakinyuki kuoneshwa kadi nyekundu.
Kwa matokeo hayo Simba SC inaendelea kuwa na alama 24 zinazoiweka nafasi ya pili, baada ya kucheza michezo 11, huku Mbeya City ikifikisha alama 19 na kukwea hadi nafasi ya tatu.
Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kumiliki alama 32, baada ya kushuka dimbani mara 12.