Kocha Msaidizi wa Klabu ya Simba SC Selemani Matola amesema maandalizi yanayoendelea Kambini Ismailia-Misri yatakua chachu kwa kikosi chao, kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Simba SC ina muda wa juma moja tangu ilipoanza kambi nchini Misri, na tayari imeshacheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao Ismailia wanaoshiriki Ligi Kuu ya Misri, na kuambulia sare ya 1-1.
Matola amesema wachezaji wote waliopo Kambini kwa sasa wameonesha kuwa tayari kwa mapambano ya msimu mpya chini ya Kocha Zoran Maki ambaye amekabidhiwa jukumu hilo baada ya kuondoka kwa Kocha Franco Pablo Martin.
“Siku chache tulizokuwa hapa Misri tumekua na mafanikio makubwa, wachezaji wameonesha juhudi kubwa kwenye mazoezi, wanajituma na kutekeleza kikamilifu kile wanachoelekezwa, naamini furaha iliyopotea msimu uliopita itarejea tena msimu ujao.” Amesema Kocha Matola
Kikosi cha kimefikisha idadi ya wachezaji 24 waliopo Kambini Ismailia-Misri, baada ya wachezaji wengine watano kujiunga na wenzao mwanzoni mwa juma hili kwenye maandalizi ya msimu mpya 2022/23.
Wachezaji ambao hawakuwa sehemu msafara wa awali ulioelekea Misri ni Moses Phiri (Zambia), Henock Inonga Baka (DR Congo), Peter Banda (Malawi), Thadeo Lwanga (Uganda) na Nassoro Kapama (Tanzania).