Kikosi cha Simba SC kimeanza kujiwinda na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaowakutanisha na Watani zao wa Jadi Young Africans, Jumapili (Oktoba 23) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC imerejea katika Uwanja wa mazoezi baada ya wachezaji kuwa katika mapumziko ya siku moja, kutokana na uchovu wa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya CD Primeiro de Agosto ya Angola uliopigwa Jumapili (Oktoba 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye Kurasa za Mitandao ya Kijamii ya Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally, imethibitika kikosi cha Mnyama kimeanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Young Africans.
Ahmed ameandika kuwa, Simba SC wanaupa uzito mkubwa mchezo huo, ambao wanahitaji kushinda ili kuendelea kujikita katika kilele cha msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo kwa sasa wana alama 13 sawa na Young Africans, lakini wakiwa na uwiyano mzuri wa tofauti ya mabao ya Kufunga na Kufungwa.
Ahmed Ally ameandika: Leo rasmi tumemaliza sherehe za kufuzu hatua ya makundi Afrika.
Sasa tunaanza maandalizi ya mchezo wetu wa ligi kuu ya NBC October 23.
Mchezo huu tunauchukulia kwa uzito wa kipekee sio kwa sababu ni derby bali tunahitaji alama tatu za kutuwekea salama kileleni.
Licha ya ukweli kuwa ni mechi ngumu sana kwetu kwa sababu tunacheza na watu ambao hii ndo mechi yao kubwa maishani.
Tunacheza na watu ambao mafanikio yao makubwa ni kucheza na sisi.
Tunaingia kwenye mchezo huu mioyo yetu ikawa na uwoga na wasiwasi kwani tumepoteza dhidi yao mara mbili.
Ni mechi ngumu sana lakini jukumu letu ni kusimama imara na kuvuna alama tatu.