Uongozi wa Simba SC umekiri kupokea kwa mikono miwili maamuzi ya Kocha Mkuu wa Taifa Stars Adel Amrouche ya kuwaacha Wachezaji Shomari Kapombe na Mohamed Hussein kwenye kikosi chake, kitakachoingia kambini mwishoni mwa juma hili jijini Dar es salaam.
Kocha Amrouche alitangaza kikosi chake jana Jumatatu (Machi 13), kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi F wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ dhidi ya Uganda utakaopigwa ugenini Machi 24.
Akihojiwa na Wasafi FM mapema leo Jumanne (Machi 14) Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema, maamuzi ya kocha huyo mpya wa Stars ya kuwaacha wachezaji hao, kwao ni sahihi kwa sababu wanawahitaji katika kipindi hiki ambacho wanaamini ni muhimu sana kwa klabu.
Amesema pamoja na kutambua uwezo wa wachezaji hao wawili katika majukumu ya kitaifa, lakini bado Kocha Mkuu ameona ni wakati wao kuwapisha wengine, hivyo nafasi hiyo wataitumia kama klabu kukaanao ili kuweka sawa mipango yao ya kushinda mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Horoya AC.
“Tumefurahi kuona Mohamed Hussein na Shomari Kapombe hawajaitwa katika kikosi cha Taifa Stars. Hii inawafanya wawe na muda mzuri wa kuitumikia Simba SC na zaidi ni katika mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya Horoya AC.”
Simba SC ina kibarua cha kusaka ushindi kwenye mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi C Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Horoya AC utakaopigwa Jumamosi (Machi 18), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam. Katika Msimamo wa Kundi hilo, Simba SC inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 06, ikitanguliwa na Raja Casablanca ya Morocco yenye alama 12, huku Horoya AC ya Guinea ikiwa nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 04 na Vipers SC ya Uganda inaburuza mkia ikiwa na alama 01.