Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Mulamu Nghambi amesema ni vugumu kwa klabu hiyo kumsajili tena Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Msumbiji na klabu ya Al Ahly ya Misri Luis Jose Miquissone.
Kiungo huyo anatajwa kuwa mbioni kuondoka Al Ahly mwishoni mwa msimu huu, kufuatia kushindwa kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wa Kocha Pitso Mosimane, aliyependekeza asajiliwe mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Simba SC.
Mulamu ametoa kauli hiyo alipohojiwa na Azam TV jana Jumatano (April 07), ambapo amesema Mshambuliaji huyo kwa sasa ni mali halali ya Al Ahly, na kama atawekwa sokoni klabu ya Simba SC itakua na wakati mgumu kumsajili kutokana na vigezo vya klabu hiyo ya Misri.
Amesema mara kadhaa klabu ya Al Ahly imekua ikiweka vipaumbele vyake inapotokea inamuuza mchezaji, na kwa uchumi wa klabu ya Simba SC kufikia vipaumbele hivyo ni vigumu, hivyo haitakua rahisi kwa Miquissone kurudu tena Msimbazi.
“Al Ahly wana vigezo vyao, wapo kibishara zaidi na ndio maana wachezaji wao wengi huuzwa katika nchi za kiarabu kwa sababu zinaweza kufikia vipaumbele vinavyowekwa na klabu hiyo,”
“Simba SC kwa sasa inaweza kumsajili mchezaji kwa kuzingatia bajeti yake, kwa vigezo ambavyo tunaweza kuvifikia, lakini kwa namna Al Ahly wanavyouza wachezaji wao kwetu itakua ngumu kugombania mchezaji na klabu zenye bajeti kubwa.” alisema Mulamu Nghambi.
Miquissone alisajiliwa Simba SC wakati wa Dirisha Dogo la Usajili mwaka 2020, akitokea UD Songo ya nchini kwao Msumbiji, na kwa kipindi chote alichokaa Msimbazi alikua msaada mkubwa katika safu ya ushambuliaji.