Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC leo Jumatatu (Januari 03) asubuhi wamesafiri kuelekea Zanzibar tayari kwa Michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Simba wameondoka Dar es salaam kwa usafiri wa boti, wakiwa na morari ya juu baada ya kuivuruga Azam FC mabao 2-1 juzi Jumamosi (Januari Mosi).
Wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Mabingwa hao wameonekana wakiwa safarini kuelekea Unguja-Zanzibar, huku taarifa zikieleza kuwa baadhi ya wachezaji ambao huenda wakasajiliwa kipindi hiki (Dirisha Dogo la Usajili) wakajiunga na kikosi hicho kwa majaribio kabla ya kusaini.
Simba SC itaanza kusaka taji la Mapinduzi 2022 keshokutwa Jumatano (Januari 05) dhidi ya Selem View ya Zanzibar.
Mwaka 2021 Simba SC ilitinga hatua ya Fainali ya michuano hiyo, lakini ilishindwa kutwaa ubingwa baada ya kupoteza kwa changamoto ya penati dhidi ya Young Africans.
Michuano ya Kombe la Mapunduzi imeanza rasmi kisiwani Unguja-Zanzibar tangu jana Jumapili (Januari 02) kwa kushuhudia Namungo FC iliichama Meli 4 mabao 2-0.