Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ Simba SC imefanikiwa kuingia hatua ya Nusu fainali ya michuano hiyo.

Simba SC wamefikia lengo hilo kwa kuifunga Dodoma Jiji FC mabao 3-0, usiku huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Nahodha na mshambuliaji wa Simba SC John Raphael Bocco ameifungia timu yake mabao mawili kipindi cha kwanza, huku mshambuliaji kutoka Rwanda Meddie Kagere akifunga bao la tatu kipindi cha pili.

Simba SC itacheza dhidi ya Azam FC kwenye hatua ya Nusu Fainali katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, mkoani Ruvuma mwezi ujao.

Nusu Fainali nyingine itachezwa mjini Tabora kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mwezi ujao.

Azam FC iliifunga Rhino Rangers ya Tabora mabao 3-1 leo jioni mjini Shinyanga katika Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.

Young Africans imefika Nusu Fainali baada ya kuifunga Mwadui FC mabao mawili kwa sifuri jana Jumanne mkoani Shinyanga, huku Biashara United ya mkoani Mara wakiivurumusha Namungo FC kwa mabao mawili kwa sifuri.

Ikumbukwe kuwa bingwa wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAFCC’ msimu ujao 2021/22.

Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara atapata fursa ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ‘CAFCL’ msimu ujao 2021/22.

RC Makalla aagiza malipo fidia ya Mto Ng'ombe yaharakishwe
TRA Dar yaendelea kuvunja rekodi, RC Makalla ateta na watendaji wa taasisi